USHAIRI

   USHAIRI                                                  

Ushairi ni mojawapo ya vipera vikuu vya fasihi simulizi. Uhairi hujumuisha vijipera kadha wa kadah kama vile shairi, maghani, nyimbo na ngonjera.
 
Hebu tushughulikie kijipera shairi:
 
Kuna aina mbili kuu za mashairi:
 
Mashairi ya arudhi
Haya ni mashairi ambayo hutungwa kwa kuzingatia kwa makini taratibu za kijadi za utunzi. Hizi ni sheria zinazopokezanwa kutoka kizazi hadi kingine. Ndipo mashairi yaliyotungwa kwa kuzingatia kanuni hizo pia huitwa mashairi ya kimapokeo.
Kanuni hizo huzingatiwa katika:

 • Vina. Sharti shairi liwe na muwala wa vina katika ubeti au shairi zima
 • Mizani: Idadi ya mizani katika mishororo hudumishwa.
 • Beti: Kila ubeti una idadi maalum ya mishororo.

Kwa kudumisha idadi sawa ya mishororo katika kila ubeti, tunapata aina zifuatazo za mashairi

 1. Tathmina: Ni shairi lenye mshororo mmoja katika kila ubeti
 2. Tathnia/ Tathnitha: Shairi la mishororo miwili katika kila ubeti.
 3. Tathlitha: Shairi lenye mishororo mitatu katika kila ubeti

 
Mf
Karibu ukumbini, usiwe mpitanjia.
tukuone hadharani,tuliondowe pazia.
usijitie kizoroni, ukumbi sio ridhia.

Hashili kifichoni,ukumbini hajangia
Bi Salma dirishsani, usidhani kakimbia.
hoodhood yupembeni, selemani karidhia.

4.Tarbia : Shairi lenye mishororo minne katika kila ubeti.
 
Mf
Mikoba yetu kwapani, yatufanya tushaini
Kitembeapo njiani, wa kushoto ukwapani
Wa kulia unjiani, wapunga ufurahani
Kwa raha zetu jamani, twajimwaga tuacheni

Nataka nikupe siri, sijesema yakirihi
Mengine ina sihiri, ya waganga na warihi
Tokea alfajiri, ulalapo wafurahi
Mikoba ina kachori, na badia za falahi

5.Takhmisa:  Shairi lenye mishororo mitanokatika kila ubeti
6.Tasdisa/ Tashlita:  Shairi lenye mishororo sita katika kila ubeti
7Ukumi : Shairi lenye mishororo kumi katika kila ubeti
 
 
Mashairi huru/ Mapingiti/ Mavue
Haya ni mashairi yasiyobanwa na kanuni za kijadi za utunzi.

 1. Shairi si lazima liwe na mishororo mikamilifu
 2. Beti hazitoshani kwa urefu
 3. Si lazima idadi maalum ya mizani katika mishororo idumishwe
 4. Si lazima shairi liwe na mpangilio maalum wa vina.
 5. Mshairi ana uhuru wa kutumia migao atakayo.
 6. Aghalabu mashairi huchanganya bahari.

                       BAHARI ZA USHAIRI
Bahari za ushairi ni sura mbalimabli za mashairi zinazotokana na mipangilio badili ya maneno, migao, vina, mizani n.k
 
Baadhi ya bahari zilizopo katika mashairi hasa yale ya arudhi ni kama:
 
Bahari kutokana na mpangilio wa vina:
 1. Mtiririko:
 
Vina vya ndani vinafanana katika shairi zima, vile vile vina vya nje vinafanana katika shairi zima
 
K.M
……………………….bu,……………………… ndi
……………………….bu,……………………… ndi
……………………….bu,……………………… ndi
……………………….bu,……………………… ndi
 
 
 
……………………….bu,……………………… ndi
……………………….bu,……………………… ndi
……………………….bu,……………………… ndi
……………………….bu,……………………… ndi

 2. Ukara
 
Vina vya nje( vya utao) vina urari katika shairi zima ilhali vina vya ndani( vya ukwapi) vina hubadilika kutoka ubeti hadi mwingine.
 
Kwa mfano
 
……………………….ba……………………… za
……………………….ba……………………… za
……………………….ba……………………… za
……………………….ba……………………… za
 
 
 
……………………….ka……………………….za
……………………….ka……………………….za.
……………………….ka……………………….za.
……………………….ka……………………….za
 3.Ukaraguni:
 
Vina vya ndani na vya nje hubadilika kutoka ubeti hadi mwingine.
KM
……………………..la……………………….. ndi
……………………..la………………………...ndi
……………………..la………………………. .ndi
……………………..la………………………. .ndi
 
……………………..mi……………………… vya
……………………..mi……………………… vya
……………………..mi……………………… vya
……………………..mi……………………… vya
 
 
…………………….ya………………………..ko
…………………….ya………………………..ko
…………………….ya………………………..ko
…………………….ya………………………..ko
 4.Masivina:
 
Vina hubadilika mshororo hadi mwingine. Kila mshororo huwa na kina tofauti na mshororo unaofuatia.
KM
 
……………………..za………………………. li
……………………. pa……………………….mi
…………………….da………………………. ka.
…………………….la………………………..vyo
 
…………………… .pe,…………………….. le
…………………….mo…………………… ..pa
…………………….ki……………………….tu.
…………………….so……………………….ti
 
Bahari kutokana na mpangilio wa maneno:
5.Kikwamba:

 
Neno moja hutumiwa katika kuanzia kila mshororo. Hata hivyo, kibwagizo hakibanwi; neno la kwanza laweza kuwa tofauti na neno linaloanzia mishororo mingine.
KM
Dunia …………………, ………………..
Dunia …………………, ………………..
Dunia …………………, ………………..
Dunia …………………, ………………..
 
 
Dunia …………………, ………………..
Dunia …………………, ………………..
Dunia …………………, ………………..
Dunia …………………, ………………..
 
 6.Pindu
 
Aghalabu utao wa mshororo wa mwisho katika ubeti  ndio ukwapi wa mshororo wa kwanza katika ubeti unaofuata, hasa katika mashairi yasiyo na kibwagizo.
Mf.
 
Ukiona vyainama, vyainama vimepigwa
Vyaumia vyakunjama, vyakunjama vimetegwa
Na mapigo yaandama, yaandama tunozugwa
Jamani uhuru wetu, lini tapopatikana?
 
Lini tapopatikana, tapopatikana wetu?
Uhuru ulio pana, pana ulotanda kwetu
Shikane bibi na bwana, bwana shujaa wa kwetu
Ukiona vyaelea, vimeundwa ufahamu.
 
 
 
Vimeundwa ufahamu, ………………
……………………..,……………….
……………………..,……………….
……………………..,……………….

Katika mashairi yaliyo na kibwagizo, aghalabu utao wa mleo hutumiwa kama ukwapi katika ubeti unaofuata. 

Mf.
Mwanangu jizatiti, jizatiti uelimike
Maisha kweli magumu, kama kifuu cha nazi
Elimu ni ngao, daima takulinda
Elimika mwanangu, nuru uipate kweli

Daima takulinda, takusetiri na mawimbi
Majabari na miamba, yote utayashinda
Utaparamia juu juu, fanaka utalamba
Elimika mwanangu, nuru uipate kweli. 

 7. Mandhuma
 
Katika bahari hii, ukwapi hutoa swali ama wazo, huku utao ukitoa jibu
 
Mf.
Tata zikishinda, hazitatuki
Unalolitenda, halinyoki
Jambo likivunda, haliongoki
 
Bahari kutokana na vigao.
8.Utenzi/ Tendi:

 
Ni shairi la kigao kimoja katika kila mshororo. Aghalabu utenzi husimulia maelezo ya maswala mazito kama vile dini, historia ya nchi n.k
 
9.Mathnawi:
 
Shairi hili lina vipande viwili katika kila mshororo.
 
Mf
Memaliza ulimwengu, sijapata fani yako
Nimeipanda mikungu, kitizama kama uko
Macho mefanya kiwingu, hayaoni kwengineko
Urudi kipenzi changu, unienzi niwe wako
 
Sisikize walimwengu, kutupa mahali pako
Siharibu pendo langu, urudi hapa niliko
Nikuenzi mboni zangu, ukijue cheo chako
Nawangiwe na machungu, moyo mesabili kwako
 
Mewapiku kwa mizungu, turufu zote ni zako
Niradhi nitiwe pingu, sirudi nyuma mwenzako
Rejea nyumbani kwangu, nichezee mbawa zako
Wewe ndie ndege wangu, simtafuti mwenzako

10.Tumbuizo
 
Shairi hili huwa na vipande vitatu katika kila mshororo: ukwapi, utao na mwandamizi
 
Kila kipande huwa na mizani minane. Idadi ya mizani katika kila mshororo ni 24.
 
Mf:
_________________8____________________8_______________8
_________________8____________________8_______________8
_________________8____________________8_______________8
_________________8____________________8_______________8
 
 
_________________8____________________8_______________8
_________________8____________________8_______________8
_________________8____________________8_______________8
_________________8____________________8_______________8
 
 11.Ukawafi
 
Shairi hili lina ukwapi, utao na mwandamizi lakini idadi ya mizani katika kila mshororo ni chini ya 24.
 
Mf
__________________4____________________6______________6
__________________4____________________6______________6
__________________4____________________6______________6
__________________4____________________6______________6
 
 
__________________4____________________6______________6
__________________4____________________6______________6
__________________4____________________6______________6
__________________4____________________6______________6
 
Bahari kutokana na mazungumzo

 12.Ngonjera
 
Wahusika wawili au zaidi hujibizana.
 
13.Malumbano
 
Kuna ubishi kati ya washairi wawili wanaopingana kwa kutoa maoni tofauti tofauti.
 
Bahari kutokana na urefu wa mishororo:
 
14.Msuko
 
Kibwagizo ni kifupi kuliko mishororo mingine.
 
Mf:
_____________________6,_________________________5
_____________________6,_________________________5
_____________________6,_________________________5
­­­­­­­­­­­___________________________8
 
 
_____________________6,_________________________5
_____________________6,_________________________5
_____________________6,_________________________5
­­­­­­­­­­­___________________________8
 
       
 15.Kikai
 
Shairi hili lina mizani 12. Aghalabu, ukwapi una mizani 4 na utao mizani 8.
 
Mf
_____________________4________________________8
_____________________4________________________8
_____________________4________________________8
_____________________4________________________8
 
 
 
 
 
Miundo mingine ya bahari hii ni kama ifuatavyo:
 
______________________6_______________________6
______________________6_______________________6
______________________6_______________________6
______________________6_______________________6
 
 
Ama:
 
­­­­­­­­­­­­______________________8_______________________4
______________________8_______________________4
______________________8_______________________4
______________________8_______________________4
 
16.Sarakani
 
Bahari hii hujumuisha zaidi ya bahari moja katika shairi moja, yaani, shairi linaweza kuwa na mchanganyiko wa tarbia, takhmisa, tasdisa nk..
 
 
 
MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA UCHAMBUZI WA SHAIRI
 

 1. Muundo

 
Eleza jinsi shairi lilivyoundwa, mpangilio wake,umbo lake. Angalia:
 

 • Beti: Idadi ngapi ya beti? Kila ubeti una mishororo mingapi?
 • Vina: Vina vya nje na vya ndani vichunguzwe. Kuna urari wa vina au la?
 • Kituo: Mshororo wa mwisho umerudiwarudiwa? ( shairi lina kibwagizo au la?) Mshororo wa mwisho umefupishwa?( bahari ya msuko)
 • Mishororo: Kila mshororo una vigao vingapi? Idadi ya mizani katika kila kigao? Maneno yamepangwaje?( chunguza mpangilio wowote maalum unaoibua dhana ya bahari fulani kama vile pindu, kikai, kikwamba, nk
 • Mizani: Idadi ya mizani katika kila mshororo?

 
 

 • Utoshelezi

 
Sharti shairi liwe na wazo linaloendelezwa. Chunguza kama  maudhui yameendelezwa na kukamilishwa kimantiki.
 

 • Muktadha

 
Mukatdha wa aina gain? Ni sifa zipi zinazojitokeza kisiasa, kiuchumi, kijamii, kikazi, nk? Muktadha hutuelekeza kwenye maudhui na dhamira. 
 

 • Falsafa ya mwandishi

 
Huu ni msimamo wa malenga kuhusu suala linalorejelewa katika shairi. Maoni yake kuhusu jambo fulani ni yapi?
 

 • Mbinu za lugha:

 
Tamathali gani za usemi zilizotumika? Malenga ametumiaje fani mbalimbali kutosheleza maudhui yake? Km, methali, takriri, istiari…
 
 
 Kumbuka kwamba:

 • Ukwapi ni kipande cha kwanza cha mshororo
 • Utao ni kipande cha pili cha mshororo
 • Mwandamizi ni kipande cha tatu cha mshororo
 • Mwanzo ni mshororo wa kwanza katika ubeti
 • Mloto ni mshororo wa pili katika ubeti
 • Mleo ni mshororo wa tatu katika ubeti
 • Kituo/ Kimalizio ni mshororo wa mwisho katika ubeti
 • Kibwagizo/ Mkarara ni kituo kilichorudiwarudiwa katika kila ubeti 

All Free
Gskool is a free website for all.
We connect students and ease the accessibility of student/teacher resources.
Join for free to enjoy all the features of this website.

Open Content
Gskool is open content. The site admin is not responsible for user posts, but has the rights to delete any post considered unnecessary.  Please ensure the content posted does not breach any-one's copyright rules.

Share and Syndicate
Whatever you want to do, Gskool allows you to save or share documents, create new topics and discussions, create virtual books and all kinds of pages.
...a better way to e-learning.

Syndicate

Syndicate content

Bookmark and Share

Gskool Inc. Is a close Associate of Utandawazi Technologies